DAIMA TAYARI KWA MAOMBI

David Wilkerson (1931-2011)

Mgogoro unapotokea, huna muda wa kujijenga katika maombi na imani. Wale wanaotumia muda wao katika chumba cha maombi pamoja na Yesu, ingawa, wako tayari kila wakati.

Wenzi wa ndoa waliandikia huduma yetu hivi majuzi katika hali iliyoonyesha kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Binti yao mwenye umri wa miaka 24 alikuwa ametoka na rafiki yake wakati mwendawazimu alipowateka nyara wasichana wote wawili. Alimuua binti yao kwa njia ya kikatili. Wanandoa hao walikuwa katika mshtuko. Marafiki na majirani zao walishangaa, “Mzazi yeyote angewezaje kuokoka aina hii ya msiba?”

Ndani ya saa hiyo hiyo, Roho Mtakatifu alikuwa amewajia wanandoa hao waliokuwa na huzuni, akiwaletea faraja isiyo ya kawaida. Bila shaka, katika siku zenye uchungu zilizofuata, wazazi hao wenye huzuni waliendelea kuuliza Mungu kwa nini, hata hivyo wakati wote huo walipata pumziko na amani ya kimungu.

Kila mtu aliyejua wazazi hao alishangazwa na utulivu wao, lakini wenzi hao walikuwa wamejitayarisha kwa wakati wao wa shida. Walijua muda wote kwamba Mungu hataruhusu jambo lolote liwatokee bila kusudi la msingi. Habari za kutisha zilipokuja, hawakusambaratika kwa sababu imani yao iliegemezwa kwenye kweli zisizotikisika.

Wenzi hao wa ndoa waliishi kupatana na maneno haya ya maandiko: “Mungu ni kimbilio letu na nguvu zetu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa, ijapokuwa nchi itatikisika, na milima ijapoondolewa katikati ya bahari; maji yake yajapovuma na kutikiswa, ijapotetemeka milima kwa mafuriko yake. Sela” (Zaburi 46:1-3).

Kwa kweli, wazazi hawa na watoto wao waliobaki walianza kumuombea muuaji. Watu katika mji wao hawakukubali, lakini wenzi hao wa ndoa waliomcha Mungu walisema na kufundisha juu ya uwezo wa Mungu wa kutoa nguvu, haidhuru wakabili nini. Watu wa mjini walitambua nguvu zao kuwa zilitoka kwa Yesu pekee. Hivi karibuni walikuwa wakisema juu ya wanandoa, “Wao ni muujiza. Hao ni watu wa kweli wa Yesu.”

Ni wangapi kati yetu wanaojulikana kwa njia sawa? Je, ni wangapi kati yetu tumejitayarisha katika chumba chetu cha maombi kwa miaka mingi ili mgogoro usituangushe? Hebu tutafute uso wa Bwana sasa na tujitie nguvu ndani yake, muda mrefu kabla ya majaribu.